"Lema amezungukwa na Polisi" - Makene

Jumanne , 17th Mar , 2020

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa Polisi wamezunguka hoteli aliyofikia Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, huku wakishinikiza uongozi wa hoteli hiyo kuwaonesha chumba alicholala Mbunge huyo.

Mbunge Godbless Lema, kulia ni Mkuu wa Idara ya Habari CHADEMA Tumaini Makene.

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital leo Machi 17, 2020, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho Tumaini Makene, amedai kuwa mpaka sasa hawajajua sababu ya polisi hao kujazana hotelini hapo.

"Lema amezungukwa na Polisi Hotel ya Regency Park, Polisi wamefika pale tangu asubuhi wanamtafuta na sababu haijajulikana na wana silaha, wamelazimisha wapelekwe chumba alicholala na uongozi wa hotel umekataa maana siyo utaratibu, kwahiyo hadi sasa wako hapo wanamngoja" amesema Makene.

Mbunge Lema leo ilikuwa afanye mkutano na waandishi wa habari, kujibu madai ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) dhidi yake.