Jumatano , 6th Mei , 2015

Mbunge wa Arusha mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema amesema kuwa atashinda tena ubunge kwa tiketi ya chama hicho, hata asipopiga kampeni.

Mbunge wa Arusha mjini kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema

Aidha amesema ni vyema wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo mbalimbali nchini kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, ili waweze kupiga kura na kuchagua wagombea wanaotaka kuongoza.

Lema amesema hata asipopiga kampeni za kutetea kiti hicho yeye bado ni mbunge na uchaguzi huu ataendelea kushinda kwani wagombea wanaopitapita kutangaza nia na baadhi yao kugawa unga, bila mboga anawafananisha na bendera zinazoendelea kupepea bila kuwa na mafanikio yoyote.

Amesema ni vyema wananchi wakajitokeza kuhakikisha daftari hilo la wapiga kura likitangazwa kufika mkoani Arusha, wanajitokeza kwa wingi kujiadikisha ili waweze kutumia haki yao siku ya uchaguzi na kuongeza idadi ya wabunge na madiwani wengi kupitia Chadema.

Lema amesema kwa jinsi anavyoona hadi sasa maandalizi ya uchaguzi mkuu yanasuasua, hivyo yawezekana daftari hilo likitangazwa kuhamia mkoani Arusha siku zinaweza kuwa chache hivyo ni vyema wananchi wakawa makini, wakisikia daftari linapita mkoa fulani wajitokeze kwa wingi kujiandikisha, ili waweze kuchagua wabunge wengi kutoka Ukawa.

Amesisitiza ni vema uchaguzi ufanyike kama ulinvyopangwa, inamaana kama uchaguzi utasogezwa mbele Rais Jakaya Kikwete anaweza kutangazwa kuendelea kuongoza nchi na kwenye Katiba pendekezwa kuna mambo yamefichwa, ikiwemo kuongezwa kipengele cha Rais kuongezewa muda na ikafanyika hivyo, kwasababu tupo wachache bungeni.

Amesema anatarajia kufanya mkutano Ijumaa ya wiki hii, ataongelea mambo mbalimbali ikiwemo suala la uandikishwaji wa daftari la kupiga kura, sambamba na kujadili jinsi fedha ya Tanzania thamani yake inavyozidi kushuka.