Ijumaa , 24th Jul , 2015

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema,(Chadema) ameibuka kidedea kwa kuzoa kura 255 sawa na asilimia 93.06 kati ya wapiga kura 274 na kuwabwaga wapinzani wake kwa mbali.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema,Chadema akihutbia wananchi katika moja ya Mikutano

Wagombea wengine katika kinyang’anyiro hicho ni Noel Olevaroya 13 sawa na asilinia 4.74 na Nsajigwa Mwakatobe aliyepata kura 6 sawa na asilimia 2.18.

Akitangaza matokeo hayo jana Msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasini, aliwapongeza wagombea wote na kusema hiyo ndio Demokrasia.

Kabla ya kuanza uchaguzi huo aliwataka wapiga kura kuchagua mtu mwenye kuhimili mikiki ya Chama hicho na atakayetumika kujenga chama na sio bora kiongozi.

Aidha alitumia nafasi hiyo kumtangaza aliyekuwa Mbunge Viti Maalum Joyce Munkya, aliyepata kura 39 kati ya wapiga kura 52 na kuitetea nafasi hiyo.

Wengine katika kinyang’anyiro cha Ubunge viti maalum ni Viola Lazaro (5), Grace Macha mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima (3), Pamela Chuwa (0), Glory Kaaya (1), Theresia Minja (1), Prisca Masawe (3) na Flora (1).

Akizungumza mara baada ya kushinda kwa kishindo nafasi hiyo mbunge Lema Aliwashukuru wapiga kura kwa kumchagua kwa kishindo na kuahidi kuendelea kukijenga chama cha Chadema.

Lema amesema amejenga chama hicho kama sasa katika kiinua mgongo chake kati ya shilingi milioni 238 walizopewa, ameambualia shilingi 945,000 kwa sababu fedha zote ametumia kujenga chama kwa kununua pikipiki na kazi za chamazingine.

Amesema mbali na hilo ni mbunge pekee aliyekaa madarakani miaka miwili na kufanikiwa kufanya mambo makubwa ya kujenga ujasili wapiga kura wake, kumwaga damu yake kwa ajili ya chama, kutekeleza ahada zake za kununua magari ya wagonjwa Ambulance na kufanikisha ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto aliyoahidi.