Jumamosi , 3rd Mei , 2014

Leo ni siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani na Tanzania inaungana na mataifa mbalimbali duniani kuadhimisha siku hii huku wito ukitolewa kwa waandishi wa habari kupigania sheria ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari Tanzania.

Keneth Simbaya Rais wa Muungano wa vyombo vya Habari Tanzania UTPC.

Rais wa Muungano wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Bw. Keneth Simbaya, amesema kuna umuhimu wa kuunganisha nguvu kwa waandishi wa habari kudai sheria hiyo ili kuweza kufanya kazi katika mazingira huru zaidi.

Simbaya amesema yamekuwepo mafanikio mengi nchini ya Uhuru wa vyombo vya habari, lakini waandishi wengi wanakabiliwa na changamoto nyingi, kama vile kutumiwa jumbe za vitisho kwa kwa njia ya simu na kutishiwa maisha yao na baadhi yao kupelekwa Mahakamani.

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa SJMC Dkt. Ayub Rioba amesema uhuru wa vyombo vya habari umesaidia kubadilisha hulka za baadhi ya watawala waliokuwa wakijiweka nafasi ya Mungu kuwa wao ni kila kitu na sasa nchi zao zimekuwa na maendeleo makubwa tofauti na nyuma.