Alhamisi , 30th Nov , 2017

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Nchini, LHRC, kimesema kimesikitishwa na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi mdogo wa Madiwani uliofanyika tarehe 26 Novemba .

Akitoa tamko la kituo hicho Kaimu Mkurugenzi wake Wakili Anna Henga, amesema, uchunguzi walioufanya umebaini mapungufu makubwa hasa vitendo vya kupigwa kwa wafuasi wa vyama mbalimbali na kutoa wito kwa serikali na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika kuhusika na matukio hayo.

 Wakili Anna amesema uchaguzi huo ulikuwa na matumizi mabaya ya vyombo vya dola, watu kupigwa, kukamatwa na kujeruhiwa na kwamba, vitendo hivyo  vimeripotiwa kufanywa na vyombo vya dola, watu wasiojulikana na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa vyama vya siasa vikiwemo CCM na Chadema,

 Amefafanua kuwa, matukio hayo yasipokemewa ni kiashiria kibaya na msingi mbaya utakaoathiri uchaguzi mwingine ukiwemo wa Serikali za Mitaa wa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.