Ijumaa , 7th Aug , 2015

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba ametangaza rasmi kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichodai kuwa kunatokana Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA kushindwa kuenzi tunu za taifa za utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi

Aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha CUF taifa, Profesa Ibrahimu Lipumba akionyesha Rasimu ya Katiba pendekezwa ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania

Akiongea leo Jijini Dar es Salaam Prof. Lipumba amesema amechukua uamuzi wa kung'atuka kutokana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushindwa kusimamia makubaliano yao.

Prof. Lipumba amesema licha ya kushiriki vikao vingi vya Ukawa lakini dhamira na nafsi yake inamsuta kuendelea kushiriki katika katika umoja huo akiwa kama mwenyekiti lakini pia uongozi wa chama chake kumuona kikwazo na hana mchango wa maana katika mapambano ya kudai haki sawa kwa wote.

Aidha Lipumba ameongeza kuwa licha ya kujitoa katika nafasi hiyo lakini bado ataendelea kubaki kuwa mwanachama wa chama hicho lakini pia atakua mshauri wa masuala ya kiuchumi katika serikali ijayo.