Lissu amkumbuka Mzee Sitta kwa hili

Ijumaa , 16th Oct , 2020

Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema kuwa marehemu Samuel Sitta ndiye aliyewahi kuwa Spika wa Bunge bora zaidi kwa kuwa aliruhusu wabunge kuongea.

Kushoto ni mgombea urais kupitia CHADEMA, Tundu Lissu, na kulia ni Marehemu Mzee Samuel Sitta wakati wa uhai wake.

Lissu ametoa kauli hiyo hii leo Oktoba 16, 2020, wakati akizungumza na wanachi wa Urambo mkoani Tabora, ikiwa ni muendelezo wa mikutano yake ya kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu Oktoba 28, katika maeneo mbalimbali nchini.

"Nyie mnafahamu mzee Sitta alikuwa ni mbunge hapa kwa miaka 30, Sitta alikuwa Spika wa Bunge, katika historia yetu ya kibunge hatujawahi kuwa na Spika wa aina ya kama marehemu Mzee Sitta, na sifa yake ni moja tu aliruhusu wabunge kusema kwa sababu ni mahali pa kusema", amesema Lissu.

Katika hatua nyingine Lissu amesema kuwa, "Nataka tuwe watu huru, rais tunamchagua wenyewe akikosea tuwe na haki ya kumsema, mbunge akikosea tuwe na haki ya kumsema, Mkuu wa wilaya na Mkuu wa mkoa wakikosea tuwe na haki ya kuwakosoa kwa sababu hawa tunaambiwa ni watumishi wetu".