Jumanne , 10th Jul , 2018

Baada ya Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mh. Kangi Lugola kudai kuwa amedhamiria kumaliza tatizo la ajali za barabarani kwa kufunga matela kwenye pikipiki, baadhi ya wanaharakati wamepingana na wazo hilo wakidai kuwa haliwezi kuwa suluhisho kwa kuwa hao madereva wengi wana elimu ndogo -

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mh. Kangi Lugola alipokuwa kwenye maonyesho ya kimataifa ya biashara maarufu kama sabasaba, Jijini Dar es salaam.

hivyo wanapaswa kuelimishwa kwanza.

Akizungumza leo kwenye kipindi cha East Africa Breakfast, kinachoruka kila siku kupitia East Africa Radio, Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano, Taasisi ya Mabalozi wa Usalama barabarani, Ndg. Agustus Fungo, amesema kuwa utafiti kuhusu ajali za barabarani zinazosababishwa na pikipiki unapaswa kufanywa kwa kina hivyo Waziri anabidi kubuni mikakati mizuri zaidi kabla ya kufikiria matela.

Mkurugenzi huyo amesema kwamba suala la pikipiki kufungwa matela saizi halipaswi kuwa kama agizo na badala yake linatakiwa kuwa kama wazo kwani badala ya kutatua tatizo, yanaweza kuongezeka mengine zaidi kwa kuwa pikipiki hizo hazikutengenezwa kwa mfumo wa kuvuta tela.

"Waziri anaonekana kwamba ana nia nzuri sana, lakini kwa hili alilolisema linahitaji utafiti wa hali ya juu. Tunaweza tusitatue tatizo bali tukaongeza tatizo. Pikipiki hizi zilitengenezwa kwa mfumo wa kubeba watu wawili siyo kuvuta matela. Sheria ya spidi inapaswa kutolewa elimu zaidi kwa watumiaji wa vyombo hivi" amesema Fungo.

Akitolea mfano mfumo huo kutumika nchini India, Bw. Fungo amesema kwamba "Wenzetu wamefanikiwa katika hili la pikipiki zenye tela kwa kuwa wameweza kuwabana watumiaji kwenye sheria ya spidi. Hivyo na sisi pasipo kutoa elimu na kuzilinda sheria, kuweka matela haiwezi kuwa mwarobaini wa ajali hapa nchini".

Kwa upande wa Katibu wa Kamati ya Madereva bodaboda Taifa,  Bw. Rashid Omar, amedai kuwa kama elimu haitatolewa vifo vitaongezeka na kwamba badala ya bodaboda kuua watu wawili kwa sasa itakuwa  inaua watu watano mpaka sita  endapo hizo tela zitaunganishwa.

Hivi karibuni akiwa katika maonyesho ya Kimataifa ya biashara maarufu kama sabasaba, Waziri Lugola alieleza mkakati wake wa kupunguza ajali za pikipiki kwa kusema kwamba, serikali inakuja na mpango madhubuti wa kupunguza kama si kumaliza kabisa ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva pikipiki.

"Bodaboda dawa yenu inachemka, Tutawafungia matela ya kubebea abiria na nyie mkae kwenye foleni kama bajaji na magari mengine. Matela haya yataleta utulivu barabarani lakini pia yatawaongezea tija kwani badala ya kubeba abiria mmoja, sasa mtapakia zaidi,” Waziri Lugola.