Jumanne , 21st Mar , 2017

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema hadi kufikia jana, imepokea maombi 156 ya madaktari wa hapa nchini wanaotaka kwenda kufanya kazi nchini Kenya.

Waziri Ummy Mwalimu

Hayo yamebainishwa na Waziri wa wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu leo Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema, serikali inatoa wito kwa madaktari wasio na ajira kuendelea kutuma maombi yao kwenda kufanya kazi kwa mkataba katika nchi hiyo jirani ya Afrika Mashariki.

Kuhusu suala la usalama, Mhe. Ummy amesema, Rais Uhuru Kenyatta, amemhakikishia Rais Dk. John Pombe Magufuli, kwamba, madaktari kutoka Tanzania watapatiwa ulinzi wa uhakika wawapo nchini Kenya.

Aidha, Mh. Ummy, amekanusha kuwepo kwa upungufu wa Madaktari kwa 75% lakini amekiri kuwepo kwa upungufu wa wataalam wa sekta ya afya kwa 51% na upungufu huo si wa kwa madaktari pekee.

Tamko hilo la serikali limetolewa siku moja baada ya Chama cha Madaktari nchini (MAT), kupinga uamuzi wa Rais Dkt. Magufuli kukubali ombi la Rais Kenyatta la kupelekwa kwa madaktari 500 kwenda kusaidia kufuatia mgomo wa Madaktari wa Kenya uliodumu kwa siku 100 ambao umedumaza sekta ya afya nchini humo.

Waziri wa  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu na mganga mkuu wa serikali Profesa Muhammed Bakari Kambi.

Amesema mwisho wa kutuma maombi hayo ni tarehe 27 Machi, 2017 na kwamba kwa sasa Tanzania haina tatizo la madaktari, bali kuna changamoto ya kuwaajiri madaktari waliopo.

"Katika kipindi cha mwaka 2013/14 hadi 2016/17 madaktari 2,439 wamehitimu. Kati ya hao serikali imeajiri 615 tu. Pia watakaoajiriwa mwaka 2017/18 hawatazidi 600 ..... Hivi sasa hatuna tatizo la uwepo wa madaktari. Changamoto yetu ni kuwaajiri tunaozalisha" Alisema Ummy

Alisema Tanzania kwa sasa ina uwezo kuzalisha takribani madaktari 1,200 kwa mwaka."