Jumatatu , 19th Sep , 2022

Wizara ya Maliasili na Utalii nchini imekubaliana na Azimio la Bunge la kuridhia itifaki ya mkataba wa Umoja wa Nchi Uhuru za Afrika wa kuzuia na kupambana na ugaidi wa mwaka 2004 lililowasiliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana

Akichagia hoja hiyo leo Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema Wizara anayoiongoza itaendelea kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyohifadhiwa kisheria yakiwemo ya Hifadhi za Taifa na Misitu yanalindwa kikamilifu ili yasitumiwe na watu wenye nia ovu wakiwemo magaidi.

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameongeza kuwa pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yaliyohifadhiwa, Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuhakikisha matokeo chanya ya kazi nzuri aliyoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, katika sekta ya Maliasili na Utalii kupitia filamu ya Royal Tour yanalindwa ili Watanzania waendelee kunufaika zaidi na matunda ya fursa za Utalii na uwekezaji. 

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Uhuru za Afrika wa kuzuia na kupambana na Ugaidi ya mwaka 2004.