Jumamosi , 11th Jul , 2020

Mgombea wa Urais wa Tanzania kupitia CCM Dkt. John Pombe Magufuli amemchagua Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM.

Samia Suluhu Hassan

Magufuli amesema katika kipindi cha miaka mitano alichofanya kazi na Mama Samia kama makamu wa Rais amejifunza mengi na ameamua kuendelea naye katika awamu ya pili.

''Katika kipindi nilichofanya kazi na Mama Samia nimejifunza mambo mengi sana na kupitia yeye nawahikikishia nitakuwa mtetezi mzuri wa wanawake. Nimekuwa nikimtuma popote hakatai kama na nyie kina Mama mkitumwa hamkatai'', amesema.

Awali Ndugu Magufuli aliwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumchagua kwa asilimia 100, ambapo wajumbe wote 1822 walimpigia kura za NDIYO.

“Wajumbe mmenipa heshima kubwa na nimebaki na deni kubwa, namuomba Mungu kura nilizozipata leo zisinipe kiburi, zisifanye nijione wa muhimu sana, bali zinipe nguvu nitumikie Watanzania wote'' - Magufuli

Akaongeza kuwa ''Kura nilizopata leo zikawe salamu kwa wasaidizi wangu kuwa wana kazi ya kutimiza shauku ya wanachama na wananchi wote, hivyo tukashirikiane kuijenga nchi yetu hii tajiri''.

Kisha akatoa ahadi ya kuwatumikia zaidi wananchi kwa kusema, ''Tupo kwenye nchi tajiri na mimi nataka kuwahakikishia kama tukisimama pamoja, nchi yetu inaweza kutoa mchango mkubwa sana duniani''.

Tazama Video hapo Chini