Magufuli ameonyesha ujasiri kwa Lissu - Lusekelo

Thursday , 14th Sep , 2017

Mchungaji Lusekelo 'Mzee wa Upako' ameendelea kuwataka watu kuwa watulivu na kuviacha vyombo vya dola kufanya uchunguzi sakata la Lissu na kudai Rais ameonyesha ujasiri mkubwa kutoa salamu za pole na kuagiza vyombo vya usalama kuchunguza sakata hilo

Mchungaji Lusekelo amedai yeye anamfahamu vizuri Rais Magufuli kuwa si mnafiki ni mtu mkweli siku zote hivyo kitendo cha yeye kuviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa jambo hilo ni wazi vyombo hivyo vitafanya kazi kuwabaini watu hao waliomshambulia Tundu Lissu.

"Rais ameonesha ujasiri mkubwa sana kwa kutoa pole kama Rais wa nchi na kama Amiri Jeshi Mkuu kwa Mh. Tundu lissu ambaye ni Mwanasheria wa CHADEMA na pia ni Rais wa chama cha wanasheria nchini, Rais ameamuru vyombo vya dola vifanye uchunguzi wa kina kujua nani amehusika na uovu aliofanyiwa mbunge wa singida Tundu Lissu, tunamuamini Rais, tunaamini vyombo vya dola, kama wao hawata lipa imani yetu kwao, Mungu atalipa imani yetu narudia kama wao hawata lipa imani yetu Mungu atalipa imani yetu maana itakuwa tuliwaamini wakatuangusha lakini siamini, nina amini Rais wa nchi amesikitika na ameumia maana katika siasa hakuna uadui wa kudumu kwa kiwango cha kumwaga damu, tusifarakane tubaki wamoja maana Tanzania itabaki bila sisi na sisi tutapita" alindika Mchungaji Lusekelo 

Mbali na hilo Mchungaji Lusekelo amedai kuwa nchi haiwezi kujengwa kwa matukio bali nchi huongozwa na itikadi, sera, shertia mbalimbali pamoja na katiba 

"Nchi haiwezi kujengwa na matukio, nchi huongozwa na itikadi, sera, sheria, katiba, fikra na utamaduni, tumebahatika sisi kama Watanzania kuwa na utamaduni ambao unatengezwa na lugha yetu ya kiswahili, ndani ya lugha yetu Kuna utamaduni, kwa sasa tuvipe nafasi vyombo vya dola vifanye kazi yake mpaka dola ituambie hususani jeshi la polisi, likisema ndio tutasema lakini siamini kama litatuangusha, namfahamu sana Rais wa nchi yetu Magufuli, kama Kuna watu ambao si wanafiki ni Magufuli, kama kuna watu wakweli ni Magufuli" Alisisitiza Lusekelo.

Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa na risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma na baadaye kupelekwa nchini Kenya kwa matibabu ambako mpaka sasa anapatiwa matibabu jijini Nairobi.