Jumatano , 28th Oct , 2020

Mgombea wa Urais kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM), Dkt.John Pombe Magufuli,  amepiga kura kwenye kituo cha kupiga kura  Chamwino huku akisema kuwa siku ya leo ni muhimu katika kukuza demokrasia.

Mgombea wa Urais kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM), Dkt.John Pombe Magufuli

Akizungumza leo mara baada ya kupiga kura mkoani Dodoma akiwa ameongozana na mkewe wake Mama Janeth Magufuli, Dkt. Magufuli amewasisitiza watanzania kuendelea kuilinda amani iliyopo nchini kwani bila amani hakuna maendeleo yoyote yatakayoweza kufanyika.

"Napenda niwapongeze Watanzania wote, hii siku ya leo ni muhimu sana katika kukuza demokrasia katika Taifa letu, niwapongeze pia wasimamizi wetu katika kituo chetu cha hapa Chamwino ambacho mimi nimepigia kura maandalizi yalikuwa ni mazuri, nisisitize amani lazima tuendelee kuitunza kwa sababu kuna maisha baada ya uchaguzi" amesema Dkt.Magufuli

Aidha Magufuli amewaomba  wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya zoezi la upigaji kura, "Nawapongeza kwa usimamizi mzuri, tujitokeze kwa wingi twende tukapige kura kwa ajili ya maamuzi ambayo kila mmoja atakuwa nayo katika moyo wake" amesema Dkt.Magufuli