Ijumaa , 27th Nov , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, amewashukuru viongozi na waumini wa dini ya kiislamu pamoja na wa dini nyingine nchini kwa kuliombea Taifa katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano na amewasihi waendelee na utaratibu huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Novemba 27, 2020, na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baada ya kuswali swala ya Ijumaa katika msikiti wa Msalato jijini Dodoma.

"Wakati najiandaa kuja kuswali nilimuaga Mheshimiwa Rais na ameniagiza nilete salamu zenu kwamba anawashukuru sana kwa kumuunga mkono, amesema kuwa mbali na viongozi hao na waumini kumuunga mkono katika awamu ya kwanza ya uongozi wake, pia walitoa ushirikiano mkubwa katika kipindi cha kampeni kwa kuendelea kuliombea Taifa hadi uchaguzi ukafanyika kwa amani",amesema Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Magufuli.

Waziri Mkuu amesema kuwa, Rais Dkt. Magufuli, amewaomba viongozi hao wa dini pamoja na waumini waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa amani na utulivu.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi hao waendelee kuwahamasisha waumini washiriki ibada mbalimbali kwa sababu, jambo hilo ni muhimu na linapaswa kufanyika kwa kuzingatia muda, pamoja na kuwasihi waumini hao kuwazoesha watoto wao kufanya ibada ili wawe watoto wema.