Alhamisi , 24th Aug , 2017

Rais John Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na taratibu za uchunguzi na uendeshaji wa mashitaka ya rushwa zinavyochukua muda mrefu na ametoa wito kwa viongozi wa TAKUKURU kufanyia kazi vita dhidi ya rushwa na ionekane ikizaa matunda haraka.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo mara baada ya kumuapisha Brigedia Jenerali John Julius Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia pamoja na viongozi wengine kutoka idara mbalimbali.

“Tukifanikiwa kupunguza rushwa kwa angalau asilimia 80, nchi yetu itafanikiwa kutatua matatizo mengi, na ni vema mtambue kuwa hatua hizi tunazochukua zimeanza kuwavutia wafadhili wengi na wawekezaji", alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameendelea kufafanua jambo kwa kusema "na mimi nikiwa kiongozi wenu nimeamua kupambana na rushwa kikwelikweli, na ninawaomba nyote mshirikiane kuondoa rushwa katika maeneo yenu ya kazi”

Rais Magufuli akimkabidhi nyenzo za kazi Brigedia Jenerali John Julius Mbungo baada ya kumuapisha kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Ikulu Jijini Dar es Salaam leo.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli amewataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi na ustawi wa jamii.

“Ukiangalia mambo makubwa tunayopambana nayo yanasababishwa na rushwa iliyosambaa kila mahali, watumishi hewa chanzo ni rushwa, dawa za kulevya ndani yake kuna rushwa, vyeti feki ndani kuna rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa, pembejeo za ruzuku ndani kuna rushwa na huko mahakamani nako ni rushwa tu”,alisisitiza Rais Magufuli.

Kwa upande wake Waziri Anjellah Kairuki na Mkurugenzi wa Utawala wa TAKUKURU Bw. Alex Mfungo wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumteua Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na wamemhakikishia kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii.