Alhamisi , 8th Dec , 2022

Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji  Dar es Salaam, wamekamata majahazi matatu yakiwa yamebeba shehena ya mafuta ya kupikia yakiwa kwenye madumu ya lita 20 yapatayo 1231, yakitokea Zanzibar kuelekea Bandari bubu Kunduchi.

Moja ya Jahazi lililokamatwa na shehena ya mafuta

Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji ACP Moshi Sokoro, amebainisha kuwa walifanikiwa kukamata mafuta Desemba 6, 2022, nyakati za jioni maeneo ya Kunduchi, wilaya ya Kinondoni mkoa wa Dar es Salaam katika Bahari ya Hindi.

ACP Sokoro amefafanua kuwa Jahazi la kwanza litambulikalo kwa jina SV. Hudallah likiongozwa na nahodha Issa Bakari (26 ) mkazi wa Bububu Kihinani Zanzibar akiwa na wenzake 4, lilikutwa na madumu yapatayo 500 ya lita 20 aina ya Royal, Jahazi la pili SV. Wabaya si wote likiongozwa na nahodha Ramadhan Hamisi (42) mkazi wa Uzi Zanzibar akiwa na wenzake 3, likiwa na madumu 351 ya lita 20, Jahazi la 3 ni SV. Bora salama likiongozwa na Mwalimu Hamisi (40) mkazi wa Uzi Zanzibar akiwa na wenzake 2, likiwa na madumu 351.

Aidha kikosi hicho kiliendelea na operesheni na majira ya usiku wakafanikiwa kukamata majahazi mengine mawili, ambayo ni SV Thamarat likiongozwa na Ramadhani Eliasi (30), mkazi wa Mwanakwerekwe Zanzibar akiwa na wenzake 4 likiwa limebeba madumu 650, na Jahazi lingine SV. Subra Ngumu likiongozwa na nahodha Juma Shaibu (51) mkazi wa Mahonda Zanzibar, akiwa na wenzie 3, likiwa limebeba madumu 500, hivyo kufanya jumla ya madumu ya mafuta yaliyokamatwa kuwa 2381.

Aidha upelelezi wa awali umeonyesha kuwa mzigo huo ulitakiwa kushuka katika bandari ya Mbweni ambapo taratibu za kulipa ushuru wa forodha zingekamilika na badala yake watuhumiwa hao walielekea katika bandari bubu ya Kunduchi ili kushusha mizigo hiyo.