Ijumaa , 28th Dec , 2018

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na Mawaziri na Makatibu Wakuu kwenye eneo la tenki la maji la kutolea huduma katika ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba badala ya ukumbi wa hazina kama alivyokuwa amepanga awali.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati)

Akiwa katika eneo la Ihumwa, Waziri Mkuu amewaagiza Mawaziri wafike kwenye maeneo ya ujenzi wa ofisi zao na watathmini uwezo wa wakandarasi wanaojenga majengo ya wizara na pale watakapojiridhisha kuwa uwezo wao ni mdogo, wawabadilishe mara moja.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Ijumaa, Desemba 28, 2018) akiwa kwenye kikao cha kazi (site meeting) na mawaziri 15 na manaibu mawaziri katika eneo la Ihumwa lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.

“Mawaziri mliopo na makatibu wakuu wote kaeni na wakandarasi wenu hapa site ili waeleze kazi hii itakamilishwa lini. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kazi hii inakamilishwa kwa wakati,” amesema.

Pia ametumia fursa hiyo kuwapa mrejesho Mawaziri juu ya changamoto alizokutana nazo jana alipofanya ukaguzi wa ujenzi kwa kila wizara.

“Nataka Mawaziri ambao ofisi zao zinajengwa wa watu wa Mzinga, wakae nao na kutathmini uwezo wao na kama mtaona hawawezi, mkabidhi kwa mkandarasi mwingine,” ameongeza Waziri Mkuu.

Ameitaja Wizara inayofanya kazi nzuri mpaka sasa, ambapo amesema,  “Wizara iliyofanya vizuri kuliko zote ni ya Utumishi, wao wako hatua nzuri. Kwa maana ya uchapaji kazi, eneo nililokuta lina wafanyakazi wengi ni magereza”.

Wakati huohuo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi alimweleza Waziri Mkuu kwamba kuna wagongaji wa kokoto ambao wamepokea fedha lakini wakaamua kufunga machimbo yao kwa sababu ya sikukuu.

“Waziri wa Madini aongee nao hawa watu ili warejee na kufanya kazi kwa sababu baadhi yao wameshapokea fedha na mahitaji ya kokoto hapa ni makubwa na aliyebakia akifanya kazi ni Nyanza Road Works peke yake,” amesema.

Naye Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alimweleza Waziri Mkuu kwamba wizara yake imetoa transforma tisa za kusaidia kupoza umeme lakini ni wizara nne ambazo zimejitokeza na kulipia line za transforma hizo.