Jumamosi , 5th Nov , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini nchini wakiwemo wa Jumuiya ya Kiislamu ya Istiqaama Tanzania waongeze juhudi katika kutoa mafunzo ya dini ili kupunguza au kuondoa kabisa mmomonyoko wa maadili unaoikabili jamii.

Waziri Mkuu Tanzania Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo Novemba 5, 2022 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jumuiya Istiqaama Tanzania uliofanyika jijini Dar es Salaam huku akibainisha kuwa hivi karibuni jamii imeshuhudia vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili miongoni mwa Watanzania.

Waziri Mkuu amesema viongozi wa dini, viongozi wa umma wana wajibu mahsusi wa kuilea jamii kwa kutoa mafundisho sahihi na endelevu ya dini ili kuiwezesha kutambua na kufuata yote yaliyo mema kama ilivyo amrishwa na Mwenyezi Mungu na kuacha kabisa yote mabaya yanayomchukiza.

“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Jumuiya ya Istiqaama na Jumuiya nyingine mbalimbali za dini ambazo zimejikita katika kutoa mafunzo ya kiroho yanayoifanya jamii kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu na hivyo kuwawezesha wananchi kuishi kwa amani.” Amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Aidha, Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa taasisi za dini nchini, kuendelea kuiunga mkono serikali katika utoaji wa huduma za jamii hususani katika kipindi hiki ambacho serikali imewekeza katika miundombinu bora ya afya, elimu na maji pamoja na ongezeko la Watumishi katika maeneo ya kutolea huduma nchini.

Awali, akizungumza kwa niaba ya waumini wenzake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Istiqamaa, Sheikh Seif Ally Seif, ameshukuru serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwa taasisi za dini huku akimpongeza Rais Samia kwa kusimamia haki upendo na kujenga umoja wa kitaifa, hivyo kuifanya nchi kuendelea kuwa katika  uelekeo mzuri.