Waziri Mkuu akizungumza na wanawake wa kimasai alipombelea kituo cha mafunzo ya mikono kilichojengwa na UNICEF, Loliondo
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Wakurugenzi wa NGO na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Amesema NGO nyingi zimekuwa zikipata bajeti kubwa ya fedha lakini masuala ya maendeleo wanayoyafanya katika eneo hilo hayalingani na bajeti halisi wanazopata.
”Loliondo pekee kuna NGO zaidi ya 30 ila zilizokuwa ‘active’ ni 15 tu kuna nini Loliondo? Na baadhi yake zinafanya kazi ya kuchochea eneo hili lisiwe na amani,”.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “watu wote wanaoshirikiana na NGO hizo zinazochafua taswira ya nchi tutawashughulikia. Mnawavalisha watoto kandambili zilizotoboka na miguu michafu kisha mnawapiga picha mnazituma kwenye mitandao na kusema umasikini wa Tanzania ndio huo. Hatutawavumilia watu wa namna hii,” amesisitiza.
Amesema NGO nyingi zimekuwa zikilalamikiwa kutokana na kufanya kazi kinyume na mikataba yake ya usajili na miongoni mwa NGO hizo ni pamoja na PWC inayopata sh. bilioni 2.5 kwa mwaka, UCRT inayopata sh. bilioni 1.5 kwa mwaka, Oxfarm Tanzania inayopata sh. bilioni 1.7 kwa mwaka.
“Nitafuatilia kwa karibu kuona kazi wanazozifanya kwani zinapata fedha nyingi kwa mwaka. Lazima tujenge nidhamu kwa wote wanaopata fedha kwa lengo la kuisaidia jamii. Wote wanaojihusisha na shughuli nje ya mikataba yao wabadilike ndani ya miezi sita. Wafuate kanuni, sheria na taratibu za nchi,” amesema.