Ijumaa , 25th Oct , 2019

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, amewataka wazazi kulea watoto wao katika mazingira mazuri ili kuwaepusha kuingia katika makundi mabaya yatakayopelekea wao kufanya uhalifu.

IGP Sirro ametoa kauli hiyo leo Oktoba 25, 2019, katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea Kata ya Igoma na Makoroboi mkoani Mwanza kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

"Ukitaka kuishi vizuri Tanzania kuwa raia mwema na usicheze na bunduki na ukicheza na bunduki utaiacha familia yako na taarifa nilizo nazo wengi waliokuwa majambazi Igoma sasa ni wakulima wa Mchicha, ningependa kuwasishi watanzania, tuzae watoto, tuwadhibiti na kuwapa elimu, kesho na keshokutwa wawasaidie watanzania, usikubali kuwa na mtoto wako mhalifu badala ya kumkumbatia na kesho akapoteza maisha yake ni vizuri ukavijulisha vyombo vya dola vikamshughulikia vizuri na kumuweka kwenye mstari" amesema IGP Sirro.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Igoma Masasi Mlagata, amesema kuwa wakazi wa Kata hiyo wamekuwa na ushirikiano mkubwa kwa Jeshi la Polisi, jambo ambalo limesaidia kupunguza uhalifu.