Jumatano , 20th Mar , 2024

Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na jitihada za ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja sehemu mbalimbali Nchini ikiwa ni pamoja na ukarabati wa kiwango cha lami barabara ya Makambako – Njombe - Songea (295km).

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe Mha. Ruth M. Shalluah amesema hayo tarehe 17 Machi 2024 alipozungumza na Kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika kipindi cha miaka mitatu kwenye sekta ya ujenzi wa barabara, madaraja na viwanja vya Ndege.

Amesema katika kipindi hicho Serikali kupitia TANROADS imeendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya Kitaifa ikiwemo ujenzi wa barabara ya itoni – ludewa – manda (km 211.42); sehemu ya kwanza itoni – lusitu (km 50) kwa kiwango cha zege ambapo ujenzi unaendelea.

Ujenzi wa Sehemu ya Pili ya Lusitu – Mawengi (Km 50) kwa Kiwango cha Zege la Saruji Mradi umekamilika kwa asilimia 98, kwa sasa mradi upo kwenye kipindi cha matazamio ya uharibifu wa mwaka mmoja Mkandarasi anaendelea na kukamilisha kazi ndogo ikiwemo kupanda nyasi, uwekaji wa alama za barabarani na ujenzi wa matoleo ya barabara.

Amesema ujenzi wa Barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete (Km 92.6) kwa Kiwango Cha Lami na Zege; Sehemu Ya Kitulo – Iniho (Km 36.3) na mizani katika kijiji cha igagala unaendelea, mradi unatarajiwa kukamilika tarehe 11 Julai, 2026 na Ujenzi wa Barabara ya Njombe (Ramadhani) – Iyayi (Km.74) umeendelea kufanyika kwa awamu ambapo jumla ya Km 19.47 tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami.

Mha. Shalluah ameeleza ujenzi wa barabara ya Njombe – Makete (Km. 107.4) kwa Kiwango cha Lami umekamilika kwa asilimia 100, na tayari Serikali imeshafanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami katika Barabara ya Chimala – Matamba – Kitulo (51), Barabara ya Mkiu – Liganga – Madaba (Km 112), barabara ya Njombe (Kibena) – Lupembe – Madeke (Mfuji – Morogoro / Njombe Border (Km.125) na Barabara ya Bulongwa – Madihani – Kidope (Km. 22.15).

Aidha Serikali imeainisha Makambako (eneo la Idofi) kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja wa magari ya mizigo ili kupunguza vikwazo vya kibiashara barabarani kwa nchi za Afrika Mashariki.