Ijumaa , 1st Jul , 2016

Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania TRA, imesema inazichunguza kampuni 300 zilizokuwa zikishirikiana na mtu anayetuhumiwa kutengeneza mfumo wa kuibia serikali fedha aliyefahamika kwa jina la Mohammed Murtaza Yusuph Ali.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Alphayo Kidata.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Alphayo Kidata, amesema kuwa kampuni nne kati ya hizo zimebainika kukwepa kodi ya shilingi bilioni 30 na zimetakiwa kulipa ndani ya siku tatu.

Kamishna Kidata amesema kuwa kampuni hizo zilishirikiana na mtu huyo kukwepa kodi kwa kupewa risiti feki za EFD's zinazojumisha kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi ya Mapato.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), Kamishna Valentino Mlowola amesema kuwa kampuni hizo zimepewa siku tatu ziwe zimekamilisha kulipa malipo hayo.