Jumatano , 15th Jul , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amemteua aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Aboubakar Kunenge, kuwa Mkuu wa Mkoa huo akichukua nafasi ya Paul Makonda.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Uteuzi huo umefanyika mara moja hii leo Julai 15, 2020, ambapo pia Rais Magufuli amemteua Joseph Joseph Mkirikiti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara na kabla ya uteuzi huo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Hanang na amechukua nafasi ya Alexander Mnyeti.

Mbali na hao Rais Magufuli pia amemteua Paul Mashimo Makanza kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na Wakuu wa Wilaya mbalimbali akiwemo Dkt Selemani Serera kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Afisa Mwandamizi wa CCM Makao Makuu na anachukua nafasi ya Deo Ndenjembi.

Wakuu wa Wilaya wengine walioteuliwa hii leo ni pamoja na Ssgt Mayeka Simon Mayeka, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Kanali Patrick Norbert Songea kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Alhaj Rajab Kundya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi na anachukua nafasi ya Kippi Warioba.

Mbali na hao Rais Magufuli amemteua Joseph Kashushura Rwiza kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu, na anachukua nafasi ya Mhandisi Godfrey Msongwe Kasekenya, pia amemteua Gharib Lingo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang pamoja na Frank Fabian Chonya kuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Ruangwa.

Mbali na uteuzi huo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt Mstaafu George Mkuchika, amewateua Makatibu Tawala wanne wa Wilaya mbalimbali hapa nchini, na wateule wote hao wanatakiwa Ikulu ya Chamwino Dodoma, kesho Julai 16, 2020.