Makonda aaga rasmi, adai mwendo ameumaliza

Jumatatu , 3rd Aug , 2020

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, leo amekabidhi rasmi ofisi kwa Mkuu wa Mkoa huo wa sasa Aboubakar Kunenge, na kusema kuwa yeye hashangazwi na maneno ya watu yanayoendelea kumuandama kwa kuamini kwamba wanaofanya mazuri siku zote ndiyo husakamwa na maneno ya watu.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 3, 2020, wakati akikabidhi ofisi hiyo na kuongeza kuwa watu wasihangaike juu ya kujua yeye ataishi wapi, bali waumie siku wakisikia amemuacha Yesu.

"Mwendo nimeumaliza, imani na kiapo changu cha utumishi nimekikamilisha kikamilifu, sasa wana Dar es Salaam mniruhusu nikapumzike kwa amani katika utumishi wangu kwa kumlea mke wangu kipenzi Maria na mtoto wangu Keagan", amesema Makonda.

Aidha Makonda ameongeza kuwa, "Ningekuwa ni Jeshini ninazo medali za kivita ni Askari mmoja aliyepo back bencher mwenye uwezo mkubwa wa kupigana vita yoyote, Mkuu wa Mkoa na Mambosasa mkihitaji uzoefu wangu ktk mapambano ya kumlinda Rais Magufuli hata kama ni saa 9 usiku nitanyanyuka".