Jumanne , 14th Mei , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda leo amefanya ziara ya ukaguzi wa athari za mafuriko ambapo amesema serikali imeanza kukarabati miundombinu iliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha ikiwemo Madaraja, Barabara, Mito na Mifereji.

RC Makonda akiwa kwenye moja ya nyumba iliyoathiriwa na mafuriko.

RC Makonda amesema, miongoni mwa maeneo yanayoboreshwa na pesa ipo tayari ni mto msimbazi wenye urefu wa Km 19 na eneo la Jangwani ambalo maboresho yake yatagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 200 ikiwa ni mkopo kutoka Bank ya Dunia.

Aidha RC Makonda amesema hadi sasa jumla ya watu wawili wamefariki kutokana na mvua ambapo amewapa pole wananchi waliokumbwa na athari za mafuriko ikiwemo wale ambao mali zao zimeharibiwa na wengine kulazimika kuyaama makazi yao.

Pamoja na hayo RC Makonda amewataka wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuhama huku akiwataka wakazi wa jiji hilo kufanya usafi katika mazingira yao ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

Katika hatua nyingine RC Makonda amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Dengue kwa kuhakikisha wanatokomeza mazalia ya mbu na kuhakikisha wanawahi vituo vya afya pindi wanapoona dalili za homa.