Jumatano , 15th Jan , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezindua mfumo wa ufuatiliaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Mkoa huo, utakaorahisisha uratibu na usimamizi wa miradi mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Mfumo huo ameuzindua leo Januari 15, 2020, na kwamba utawawezesha viongozi pamoja na wasimamizi katika ngazi zote, kupata taarifa za maendeleo kidigitali kwani mfumo huo utakuwa ukikusanya na kuchakata taarifa zote na kuachana na mfumo wa awali.

"Taarifa za miradi ya maendeleo na ile ya kimkakati zimekuwa zikiwasilishwa mkoani kwa njia ya kawaida na wakati mwingine haziwasilishwi kwa wakati pale zinapohitajika, wakati mwingine zinakuwa hazina uhalisia, hivyo mfumo huu utaleta taarifa kamilifu za miradi kwenye viganja vya wasimamizi" amesema Makonda.

Aidha Makonda amesema kuwa kwa mwaka 2020, jumla ya miradi mipya  57 itatekelezwa ndani ya Mkoa huo.