Makonda kukutana na wadada walioumizwa kimapenzi

Jumatatu , 12th Aug , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amesema Serikali ya Mkoa imejipanga kukutana na wadada wote wa mkoa huo, walioumizwa baada ya kuahidiwa kuolewa na kisha mwanaume kuingia mitini na kuangalia ni njia gani nzuri zaidi ya kuwaokoa na janga hilo.

Makonda ameyabainisha hayo leo Agosti 12, 2019  kwa madai ya kwamba amekuwa akikutana na malalamiko mengi sana kutoka kwa wadada wa mkoa huo kwamba wamechoka kutapeliwa.

''Tunaompango mzuri tu wa kukutana na wadada walioumizwa,  huwezi kuwa kiongozi afu unaongoza watu walioumizwa na kutapeliwa na vijana ambao wanaona raha tu, tunataka tufikie hatua mtu akioa anaandika kwenye database ya mkoa,  ili mwanamke akitaka kuolewa anaangalia huyu jamaa kaoa au hajaoa'' amesema Makonda.

Makonda ameongeza kuwa,  wanaoumizwa wengi ni kina dada kwa sababu wanawake wakipenda huwa wanapenda kweli na wao kuwa wahanga wakubwa wa matapeli.

Amesema mkutano wa SADC wanataka kuutumia kujifunza mambo mbalimbali,  ikiwemo suala la wadada kutapeliwa juu ya masuala ya ndoa, kwa kuangalia nchi zingine zinashughulika vipi na masuala hayo.

Wakuu takribani 16 wa nchi wanachama wa SADC, wanakutana hapa nchini kwenye mkutano wa 39 wa SADC, ambapo Rais Magufuli atakabidhiwa rasmi kijiti cha Uenyekiti wa SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao