Alhamisi , 19th Dec , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema kuwa mara baada ya kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya ghorofa moja ya Chama cha Mapinduzi kinondoni, angependa kumpunguzia gharama za kupanga, Mwenyekiti wa Taifa CHADEMA, Freeman Mbowe na kumhamishia kwenye Ofisi ndogo za CCM wilayani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Makonda ameyabainisha hayo leo Disemba 19, 2019, wakati akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Jengo la ghorofa moja la Ofisi za Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi, Wilaya ya Kinondoni, jengo ambalo linatarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi bilioni 2.

"Badala ya Kaka yangu Mbowe kuendelea kulipa kodi pale Ufipa, basi tumpe hili Jengo dogo ambalo wewe Mwenyekiti wa CCM Kinondoni utaondoka, amekuwepo miaka 15 na bado ni mpangaji na jana wamemchagua tena ataendelea kuwa mpangaji, muachie akae hapa na Wajumbe wake wa Kamati Kuu, wakati anajipanga kwa sababu bado anaendelea kulipa gharama kwenye Ukumbi, badala ya kuwa na jengo lake" amesema Makonda.

Makonda amesema kuwa ujenzi wa ofisi hiyo ni mkakati wake wa kujenga ofisi nyingine kama hizo, kwenye Wilaya zote tano za Mkoa huo kwa lengo la kuhakikisha viongozi wa chama wanafanya kazi katika mazingira bora.