
Wananchi wa Malawi wanatazamia uchaguzi wa rais Jumanne wiki ijayo wakati taifa hilo likikabiliana na mzozo wa kiuchumi.
Ikiwa ni moja ya nchi maskini zaidi barani Afrika, Malawi inakabiliana na mzozo wa kiuchumi, uhaba wa chakula na mafuta na kumbukumbu za kura iliyopigwa miaka sita iliyopita ambayo ilifutwa na kuamriwa kufanyika upya kwa sababu ya dosari zilizoenea.
Mfumuko wa bei na gharama ya maisha imepanda sana, na kuna uhaba mkubwa wa mafuta na sukari. Kimbunga Freddy mnamo 2023 na ukame uliochochewa na El Niño mnamo 2024 uliharibu mazao na kuzidisha uhaba wa chakula.
Rais aliye madarakani Lazarus Chakwera, aliyekuwa mkufunzi wa theolojia na mhubiri, alikuwa mpinzani katika uchaguzi wa 2019 ulioshuhudia ushindi wa Peter Mutharika wakati huo, lakini ukabatilishwa na mahakama ya juu zaidi nchini humo.
Mwaka uliofuata, Chakwera alishinda marudio ya uchaguzi. Wakati huu, Chakwera, 70, wa Chama cha Malawi Congress anawania muhula wa pili. Mutharika, 85, wa chama cha Democratic Progressive Party, anatarajia kurejea katika uongozi pia.
Miaka mitano iliyopita, ushindi wa Chakwera hatimaye ulikuja baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya mitaani kumuunga mkono. Lakini mambo yamebadilika baada ya miaka mitano ngumu na kura hii inafanyika huku kukiwa na msukosuko wa kiuchumi na imani tete kwa taasisi za umma katika taifa hilo la kusini mwa Afrika lenye watu milioni 21.
Wawili hao wanaonekana kuwa wagombea wakuu katika uchaguzi wa Jumanne, ambao una safu ya wagombea urais 17, akiwemo rais mwingine wa zamani, Joyce Banda. Wamalawi pia watachagua wabunge katika Bunge na zaidi ya wajumbe 500 wa baraza la mitaa.