Jumatatu , 20th Apr , 2020

Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto, Askofu Gertrude Rwakatare amefariki Dunia Alfajiri ya leo ya Aprili 20, 2020.

Askofu Gertrude Rwakatare, wakati wa uhai wake

Taarifa hiyo imetolewa na Mwanaye Mutta Rwakatare, wakati akizungumza na Supa Breakfast ya East Afrika Radio.

"Ni bahati mbaya imetokea asubuhi ya leo saa 11 kasoro, alikuwa na matatizo ya moyo, jana tulimkimbiza Hospitali lakini bahati mbaya imetokea, tupo katika hatua ya kuangalia namna gani tutafanya ili tuweze kumpumzisha mama yetu" amesema Muta.

Mama Rwakatare alizaliwa Disemba 31, 1950, na hivyo amefariki akiwa na umri wa miaka 70.

Ikumbukwe kuwa Mama Rwakatare aliwahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Mvomero kuanzia mwaka 2008 hadi 2015, na baadaye mwaka 2017 aliapishwa na Spika wa Bunge Job Ndugai, kama Mbunge wa kuteuliwa na Rais wa kipindi hicho Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.