Ijumaa , 22nd Mar , 2024

Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Sheikh Husein Maneno Simo ametoa wito kwa Waislam wote nchini kuendelea kulinda amani iliyopo na kuwa wazalendo.

Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Sheikh Husein Maneno Simo

Sheikh Huseni ameyasema hayo leo, katika Msikiti wa Azhar uliyopo Kata ya Kivinje Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ambapo amewataka Waislamu wote kujivunia amani iliyopo nchini na  kuwataka watende matendo mema ambayo yanamfurahisha Mwenyezi Mungu.

“Katika Mwezi wa Ramadhani Waislam wote wanatakiwa kutosema maneno machafu, kutokufanya matendo maovu ambayo  yanahatarisha amani ya nchi na matendo mengine ambayo uislamu haukubaliani nayo ’’alisema Sheikh Huseini. 

Alisisitiza kuwa uislamu ni dini ambayo kwa sehemu kubwa inahimiza amani kama ilivyo jina lake al islam lenye maana ya  amani.

“Hivyo sisi kama Watanzania kama wanakilwa na kama waislamu ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba amani ya Tanzania inakuwa kipaumbele na amani ya Kilwa inakuwa kipaumbele’’ alieleza Sheikh Huseini.

Pamoja na hayo, ameongeza Serikali hivi saaa inatengeneza miundombinu kwaajili ya kuwasaidia wananchi lakini  uharibifu unafanywa na mingoni mwetu hivyo ni wajibu wa kila muislamu kutumia mwezi wa ramadhani kutenda matendo mema na kuwa mzalendo wa taifa hili.