
Kundi la Sudan Liberation Movement limesema maporomoko makubwa ya udongo kwenye eneo la Darfur Magharibi nchini Sudan, yamesababisha maafa makubwa yakifunika vijiji na kuua watu zaidi ya 1,000.
Maafa haya yamejiri baada ya siku kadhaa za mvua kubwa na kijiji cha Tarasin kilichoko katika milima ya Marra kimefunikwa chote kwa mujibu wa waasi hao. Kundi hilo limetoa wito kwa umoja wa Mataifa na mashirika mengine, kuwasaidia raia walioathiriwa ikiwemo operesheni za uokoaji na utafutaji wa miili ya watu waliofunikwa na vifusi vya udongo.
Wakati huohuo, sehemu kubwa ya jimbo la Darfur, ikiwa ni pamoja na eneo ambako maporomoko ya ardhi yameripotiwa, mashirika ya kibinadamu yameshindwa kufika kutokana na mapigano yanayoendelea, na hivyo kuzuia kwa kiasi kikubwa utoaji wa msaada wa dharura.
Sudan inakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, vita ambayo imeiingiza nchi hiyo katika moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Licha ya kundi la SLM kujitenga na mapigano yanayoendelea, lakini linadhibiti sehemu kubwa ya safu ya milima mirefu zaidi nchini Sudan.