Marais 19 kuwasili Tanzania

Jumatano , 12th Jun , 2019

Waziri wa Mambo ya Nje Profesa Palamagamba Kabudi amebainisha takribani Marais 19 kutoka nchi za Jumuiya ya SADC wanatarajiwa kuwasili nchini, wakiambatana na jumla ya wageni 1000, kwa ajili ya kushiriki mkutano wa jumuiya hiyo.

Waziri Kabudi ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari, juu ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa SADC unaotarajia kufanyika Agosti 17, na 18 mwaka huu.

Akitoa ujumbe huo kwa waandishi wa habari Waziri Kabudi amesema kuwa "2019 Tanzania itakuwa Mwenyekiti na mwenyeji wa mkutano wa 39 wa SADC utakaofanyika Agosti 17 na 18, na utatanguliwa na vikao vya awali kati ya Makatibu Wakuu na Mawaziri wa SADC, pia kutakuwa na maonesho ya wiki ya viwanda kwa nchi za SADC kuanzia 22 hadi 26 Julai 2019, Wakuu wa nchi 19 watakuwepo hapa, jumla ya wageni watakuwa 1000"

Mara ya mwisho Tanzania kuongoza Mkutano huo ulikuwa mwaka 2003, katika kipindi cha utawala wa Rais Mkapa ambapo mkutano hu mara nyingi umekuwa ukilenga kujadili masuala ya kiuchumi yanahusu nchi hizo.