Alhamisi , 18th Feb , 2016

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe. Charles Kitwanga amewataka makamanda wote wa Jeshi la Polisi wa mikoa kuweka mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu katika himaya zao.

Kitwanga ametoa agizo hilo ili kupunguza uwezekano wa wahalifu kukimbilia katika maeneo mengine pindi wanapofanya uhalifu.

Waziri Kitwanga ameyasema hayo leo wakati akifungua mkutano uliowakutanisha maafisa waandamizi wa jeshi la polisi nchini na kubainisha kuwa serikali imejipanga kikamilifu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili jeshi hilo

Amesema miongoni mwa mikakati ya serikali ni pamoja na kujenga nyumba zaidi ya elfu tatu kila mwaka na kuboresha mishahara ya maaskari ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa.

Aidha, Mhe. Kitwanga amewataka makamishna hao kuongeza nguvu katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa wafanyabiashara wakubwa ambao wanafadhili biashara hiyo ambapo vita hiyo inahitaji umakini mkubwa katika kupambana nayo na si kuwabana watumiaji pekee.