Jumanne , 17th Feb , 2026

Licha ya ushindi wa kikatiba uliopatikana hivi karibuni mkoani Mwanza, ambapo Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mwanza ilibatilisha sheria inayompa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mamlaka ya kipekee ya kulinda mashahidi kwa siri, kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, it

Licha ya ushindi wa kikatiba uliopatikana hivi karibuni mkoani Mwanza, ambapo Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mwanza ilibatilisha sheria inayompa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mamlaka ya kipekee ya kulinda mashahidi kwa siri, kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, itaendelea kutumia utaratibu huo wa 'vificho' kwa muda wa mwaka mmoja ujao.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu, uliotolewa Februari 16, 2026, umeweka wazi kuwa Kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinakiuka Katiba kwa kuleta ubaguzi, lakini uamuzi huo hautasitisha matumizi ya vifaa vya kumficha shahidi katika kesi ya Lissu kwa sasa.

Wakili Fulgence Massawe, Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu kesi hiyo. Ingawa mahakama imekubali kuwa sheria hiyo "inajeruhi" misingi ya haki ya kusikilizwa (Fair Trial), haikuifuta mara moja.

Mahakama imeipa Serikali na Bunge miezi 12 (hadi Februari 2027) kurekebisha kifungu hicho. Katika kipindi hiki, sheria hiyo inaendelea kuwa na “uhai wa kisheria”. Kwa kuwa sheria bado ina nguvu, kesi ya Tundu Lissu, ambayo tayari imekuwa ikitumia utaratibu wa mashahidi wa kificho, itaendelea bila mabadiliko yoyote ya kiufundi.

“Kwahiyo mfumo wetu wa kijinai umekuwa ni wa tatizo kubwa na ndivyo ulivyo na kwa bahati mbaya mahakama haikubatilisha ‘outright’ kile kifungu, huenda kama wangesema kwamba kile kifungu ni void ab initio (batili tangu mwanzo) toka jana ile ile waliposoma ile hukumu ilibidi wavunje kile kizimba na watafute njia nyingine ya kuendelea na kesi ya Tundu Lissu, labda waiahirishe mpaka warekebishe sheria au waachane nayo au wasiwe na mashahidi wa vificho", ameeleza Wakili Massawe kupitia Clubhouse.

Hivi sasa, kesi ya Tundu Lissu inaendelea huku mashahidi wa upande wa Jamhuri wakitoa ushahidi kwa usiri mkubwa. Chini ya kanuni za mwaka 2025, mashahidi huwekwa kwenye kizimba maalumu ambacho majaji na mawakili wa DPP pekee ndio wanaoweza kuwaona, Mshtakiwa (Lissu) anasikia sauti ya shahidi lakini hawezi kumtambua kwa sura wala jina.