Ijumaa , 13th Mei , 2022

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju ameyataka Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) 4909 nchini kuwasilisha maelezo ya kwanini yasifutiwe usajili kwa kukiuka sheria na taratibu zinazo yaongoza.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju

Mpanju ametoa agizo hilo alipokutana na NGOs za Mkoa wa Iringa katika ziara yake ya siku mbili mkoani humo yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

Mpanju amesema kuwa, Mashirika hayo yameshindwa kutekeleza matakwa ya kisheria inayowataka kuwasilisha taarifa zao kwa ajili ya uhakiki, lakini tangu zoezi la uhakiki lianze mwaka jana mashirika hayo yameshindwa kufanya hivyo.

"Hadi zoezi linakamilika mwezi Machi mwaka huu ni Mashirika 4864 kati ya 12884 yamehakikiwa na mashirika 7533 ndiyo yapo hai baada ya zoezi la uhakiki, sasa niwaombe NaCONGO hakikisheni yale mashirika ambayo hayakuhakiki kwa kipindi cha mwaka mmoja yaeleze sababu kwa nini yasifutiwe ndani ya mwezi mmoja, hapa Iringa ni mashirika 79 kati ya 170"q amesema Mpanju.