Alhamisi , 9th Jan , 2020

Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), limefuta matokeo yote ya watahiniwa 333, waliofanya udanganyifu katika mitihani yao, ukiwemo mtihani wa upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne(SFNA), mtihani wa kidato cha Pili (FTNA) na kidato cha Nne (CSEE).

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA). Dkt Charles Msonde.

Akitangaza matokeo hayo leo Januari 9, 2020, Jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt Charles Msonde, amesema kuwa katika matokeo ya mtihani wa upimaji kwa wanafunzi wa kidato cha Pili, umeonesha kuwa hawakufanya vizuri katika masomo matatu ikiwemo, Basic Mathematics, Chemistry na History.

"Kati ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganifu, watahiniwa 142 ni wa Darasa la Nne, 29 ni wa kidato cha Pili na 162 ni wa kidato cha Nne, ambapo pia tumezuia matokeo ya watahiniwa 538, ambao walipata matatizo ya afya na wote walipata fursa ya kufanya tena mitihani kwa masomo ambayo hawakufanya" amesema Dkt Msonde.

Aidha katika matokeo hayo jumla ya watahiniwa 340,914 wa kidato cha Nne waliofanya mitihani yao kwa mwaka 2019 sawa na asilimia 80.65, kati ya watahiniwa 422,722, wamefaulu.