Ijumaa , 16th Dec , 2016

Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya limetoa taarifa ya uhalifu mkoani humo kwa kipindi cha Januari 2016 hadi Desemba 2016 ambapo hali ya uhalifu kwa makosa yote ya jinai makubwa na madogo imepungua kwa asilimia 1.4 huku ajali zikipungua kwa asilimia 19.

Dhahiri Kidavashari - Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoani humo Dhahiri Kidavashari inaonesha kuwa makosa yote ya jinai yaliyoripotiwa katika kipindi cha mwaka 2016 yalikuwa ni 22,079 ikilinganishwa na makosa 24,833 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2015.

Amesema kati ya  makosa hayo yote,  makosa makubwa yalikuwa 1,977  wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 makosa makubwa yalikuwa 2,083 na makosa madogo yalikuwa 20,102 wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 yalilipotiwa matukio 22,750.

Makosa yatokanayo na jitihada za Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine kupitia misako/doria kwa mwaka 2016 yalikuwa 620, wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 yalikuwa 605.

Sehemu ya jiji la Mbeya

Kwa upande wa makosa ya  usalama barabarani, jumla ya  makosa  yote ya  ajali pamoja na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2016  yalikuwa 60,778, wakati kipindi kama hicho  mwaka 2015 makosa 56,798 yaliripotiwa.

Amesema pesa zilizokusanywa kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani mwaka 2016 zilikuwa Tshs 1,775,970,000/= wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 zilikusanywa pesa Tshs 1,142,870,000/

Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismas na mwaka mpya ikiwa kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyopo katika maeneo yao