Jumanne , 5th Jul , 2016

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga marufuku uvutaji wa shisha ambao umezoeleka sana mijini na katika maeneo mengi ya starehe kwa maelezo kwamba inaharibu vijana wengi kutokana na vitu vinavyochanganywa humo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku matumizi ya shisha akimuunga mkono Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ambaye mara kadhaa alitangaza kupinga matumizi hayo.

Kufuatia maagizo hayo East Africa Radio imezungumza na Daktari Nassoro Ally kutoka hospitali ya Temeke Jijini Dar es salaam na kuthibitisha kwamba shisha sii salama kwa matumizi kwani huharibu afya ya mtumiaji.

‘’Kiwango cha tumbaku inayowekwa mle na kuchanganywa na vitu vingine ili kuleta ‘fleva’ haina kiwango tofauti na sigara ya kawaida ambayo ina kiwango’’- Amesema Dkt. Nassoro.

Aidha Dkt. Nassoro amesisitiza kuwa moshi unaovutwa ni mwingi sana kiasi kwamba wavutaji moshi mwingine hutokea masikioni , ambapo mapafu huathirika kwa kiasi kikubwa.