Alhamisi , 27th Oct , 2022

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, ametoa rai kwa mamlaka za upangaji wa matumizi ya ardhi nchini kubainisha maeneo ya kilimo na kuwapanga vizuri wakulima ili kupunguza migogoro ya ardhi inayosababishwa na mahitaji ya shughuli za kilimo na hivyo kupelekea uvamizi kwenye maneo.

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde

Naibu Waziri Mavunde ameyazungumza hayo katika mkutano wa wananchi wa Kijiji cha Kibengula, wilayani Mufindi mkoani Iringa wakati wa ziara ya kamati ya mawaziri 8 wa kisekta ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya vijiji 975 nchini.

"Kilimo ni shughuli ya uzalishaji mali ambayo hitaji lake kubwa ni ardhi na ni dhahiri kwamba asilimia kubwa ya Watanzania wanakifanya kilimo kama shughuli yao kuu ya kiuchumi," amesema Naibu Waziri Mavunde.

Mavunde ameongeza kuwa, "Utambuzi na upangaji huu utasaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi hasa kwa wakulima na wafugaji, lakini pia itasaidia kupunguza uvamizi katika maeneo ya hifadhi za misitu kama ambavyo inatokea hivi sasa".

Aidha Mavunde amesema, serikali inaendelea na zoezi la kupima afya ya udongo nchi nzima ili kusaidia kuwapa wakulima taarifa sahihi ya ikolojia ya maeneo yao ya kilimo juu ya aina ya mazao ya kupanda na aina ya mbolea za kutumia.