
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio baada ya kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov. Trump amethibitisha taarifa hiyo akisema haitaji kuwa na mkutano usio na tija wala kupoteza muda.
Urusi kwa upande wake imesema maandalizi ya mkutano huo kati ya Trump na Putin yanaendelea lakini kwanza kunahitajika kukubaliana katika mambo kadhaa muhimu. Ikulu ya Kremlin imetoa tangazo baadaye na kusisitiza kuwa masharti yake ili kufikia amani nchini Ukraine bado hayajabadilika.
Donald Trump amesema hataki "mkutano wa kupoteza muda" baada ya mpango wa mazungumzo ya ana kwa ana na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kuhusu vita vya Ukraine kuahirishwa.
Rais Trump amedokeza kuwa kukataa kwa Urusi kusitisha vita katika maeneo ya mipaka na Ukraine ndilo suala tete linalofanya mazungumzo kuwa magumu kufanyika.
Hapo awali, afisa wa Ikulu ya White House alisema "hakuna mipango" ya mkutano wa Trump-Putin "katika siku za usoni", baada ya Trump kusema Alhamisi kwamba wawili hao watafanya mazungumzo huko Budapest ndani ya wiki mbili.
Tofauti kuu kati ya pendekezo la Marekani na Urusi kwa ajili ya amani ilizidi kuonekana wazi wiki hii, na kuonekana kupoteza nafasi ya mkutano wa kilele.
Uamuzi wa White House wa kuahirisha mipango ya mkutano wa pili wa Trump na Putin unaweza kuonekana kama jaribio la kuzuia hali nyingine kama hiyo.