Mbowe aeleza anavyomfahamu Ndugai "Muombeeni"

Jumapili , 17th Mei , 2020

Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amewaomba Watanzania kumuombea sana Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai kwa kuwa anaenda kumaliza kipindi chake cha mwisho cha wadhifa huo.

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe.

Mbowe ameyabainisha hayo leo Mei 17, 2020, wakati akizungumza Mubashara, na kuonesha kushangazwa na namna ambavyo Spika Ndugai amekuwa akimuongelea Bungeni kwa wiki mbili mfululizo, licha ya kwamba wote wamesoma Shule moja, na wamekuwa pamoja Bungeni kwa kipindi cha miaka 20.

"Mh Spika anajua vizuri sana kwamba tumekutana Bungeni miaka 20 iliyopita, anatambua ninamheshimu, mimi binafsi sijawahi kumvunjia heshima hadharani wala sirini,  tumekuwa wote katika kamati mbalimbali na wengine pengine hawajui, Mh Ndugai amesoma Kibaha Sekondari na mimi hapo, huyu ni Schoolmate wangu na naliomba Taifa, kumuombea Mh spika, ambaye anakwenda kumaliza muda wake hivi karibuni" amesema Mbowe.

Aidha Mbowe ameongeza kuwa wao kama chama, wameamua kuwaza kizazi kijacho, badala ya kuwaza uchaguzi ujao.