Alhamisi , 22nd Jul , 2021

Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limethibisha kuwakamata viongozi 15 wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho taifa Freeman Mbowe, na kusema Mbowe yupo Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kufuatia kuwa na tuhuma nyingine katika mkoa huo.

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi, amesema kiongozi huyo wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini alitiwa mbaroni alfajiri ya kuamkia jana Jumatano Julai 21 akiwa hoteli ya Kingdom mkoani humo, na kwamba viongozi wengine wa chama hicho wanaendelea kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza.

"Baada ya kumkamata, wenzetu wa Dar es Salaam nao walitueleza kuwa wanamtafuta kwa makosa mengine anayodaiwa kuyafanya huko, hivyo tulimsafirisha kwenda Dar es Salaam anakoendelea kuhojiwa," amesema Kamanda Ng'anzi.

Aidha, Kamanda Ng'anzi ameongeza kuwa mara baada ya mahojiano yake na Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam, atarejeshwa Mwanza ili aungane na wenzake wanaoshikiliwa kuhusiano na Kongamano la Katiba mpya ambalo hapo jana lilizuiliwa kufanyika.