Jumanne , 4th Aug , 2020

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA Jimbo la Bukene Lumola Kahumbi, aliyejitambulisha kama mdogo wake na Waziri Kigwangalla amesema, amezunguka kwa siku 11 maeneo tofauti na kukutana na wananchi kwa ajili ya kuwahoji, ambapo wengi walitamani chama hicho kimteue Tundu Lissu kugombea Urais.

Kushoto ni Lumola Kahumbi na kulia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamis Kigwangalla.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, ambapo Lumola amesema kuwa wananchi wengi hawawatambui wagombea wengine zaidi ya Lissu, kwa kuwa wanamuona ndiye anaendana kisiasa na mgombea wa nafasi ya Urais kupitia CCM Dkt Magufuli.

"Mimi ni mdogo wake Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Kigwangalla, nilianza safari ya kuzunguka maeneo tofauti na nimefikia watu 1500, lengo lilikuwa ni kuwauliza wanachi wangetamani CHADEMA katika nafasi ya Urais wamsimamishe nani, ambapo kwa maoni yao walitamani awe Tundu Lissu, nguvu ya upinzani inahitajika sana katika kuyapata mageuzi katika nchi na  wananchi wengi hawawajui wagombea wengine zaidi ya Lissu na wanaona ndiye mtu pekee anayeweza kuendana na siasa za mgombea wa CCM", amesema Lumola.

Tazama video hapa chini