Jumapili , 4th Jan , 2015

Jeshi la polisi mkoani Katavi limefanikiwa kudhibiti uhalifu na kukamata vipande 22 vya meno ya Tembo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 157.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku chache baada ya jeshi hilo kuimarisha ulinzi na doria katika sherehe za mwisho wa mwaka ikiwemo krismas na mwaka mpya,

Akiongea mjini mpanda, wakati akitoa tathimini ya matukio ya uhalifu yaliyotokea wakati wa sherehe hizo za krismas na mwaka mpya, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari amesema ushirikiano kati ya wananchi na jeshi la polisi umesaidia kudhibiti uhalifu na kufanikisha kukamatwa kwa vipande hivyo vya meno ya Tembo.

Amesema vipande hivyo vilikuwa vinasafirishwa kutoka Mpanda kwenda mkoani Kigoma vikiwa vimepakiwa kwenye basi la kampuni ya Adventure.

Amesema kuwa hii ikiwa ni mara ya pili kwa basi hilo kukamatwa na meno ya Tembo na kwamba katika tukio hilo watu watatu walikamatwa kuhusika na usafirishaji wa nyara hizo ambao umesababisha vifo vya Tembo saba na mpaka sasa basi hilo limezuiliwa na jeshi la polisi mkoani Katavi kwa uchunguzi zaidi.

Aidha kamanda wa polisi mkoani Katavi Dhahiri kidavashari ametoa wito kwa wananchi kuendeleza ushirikiano na jeshi la polisi ili kuimarisha hali ya ulinzi na kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Pia amewataka wananchi kuishi kwa kuzingatia maadili mema katika jamii na kumuogopa mungu hatua ambayo amesema itasaidia kupunguza uhalifu ukiwemo ujambazi.

Amemaliza kwa kusema kwamba polisi imeweka mikakati endelevu ya kukabiliana na matukio mbalimbali ya uhalifu yakiwemo ya kutumia silaha katika mkoa wa Katavi kwa mwaka mzima wa 2015.