Jumatano , 27th Dec , 2017

Meya wa Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, Raymond Mboya amekanusha tetesi za kujivua wadhifa wake na kuhama CHADEMA kisha kuhamania CCM na kufafanua kwamba wanaofanya hivyo hawazitendei haki kazi ambazo wamepewa na wananchi.

Mboya ambaye ni diwani wa Kata ya Longuo ametajwa kwamba ana lengo la kukihama chama hicho, lakini amekanusha na kusema kuhama chama na kuacha kazi sio kuunga mkono Serikali bali ni kuchezea rasilimali za nchi.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake amesema kwamba  taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kutaka kuhama chama sio za kweli na wananchi wapuuze.

“Kila mmoja anaunga mkono Serikali lakini sio kwa kuacha kazi na kumuunga mkono mtu anayefanya kazi. Tumechaguliwa na wananchi ili tuwatumikie na sio wametuchagua ili tuharibu rasilimali,”amesema Mboya.

Hata hivyo alisema katika kuunga mkono sera ya viwanda,Manispaa ya Moshi inatarajia kuanzisha kiwanda kidogo cha mbolea inayotokana na takataka zinazozalishwa na wakazi wake.

Amesema kiwanda hicho kitaanzishwa kwa kushirikiana na serikali ya Ujerumani na kitajengwa katika eneo la dampo kuu la takataka ambalo liko Kaloleni.

Amesema zaidi ya tani laki mbili za takataka huzalishwa kila siku na katika upembuzi wa awali takataka hizo zinatosha kuanzisha kiwanda hicho.