Alhamisi , 29th Sep , 2022

Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Umoja wa Falme za Kiarabu umeahidi kutoa mkopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania

Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa umeme wa Benaco-Kyaka, mkoani Kagera na ujenzi wa makazi ya watumishi ya gharama nafuu Visiwani Zanzibar, inayokadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 420. 

Ahadi hiyo imetolewa Mjini Abu Dhabi na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Makao Makuu ya Mfuko huo, mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Mohammed Saif Al Suwaidi alimweleza Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa miradi mingine ya kimkakati iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania kwenye Mfuko huo ukiwemo wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere na Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) itatafutiwa ufadili kupitia Serikali pamoja na Sekta Binafsi ya nchi hizo kwa kuwa inahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo wa Abu Dhabi Fund, Mhe. Suwaidi, alisema kuwa Mfuko wake uko tayari kusaidia pia utekelezaji wa miradi mingine ya kilimo na uvuvi na kwamba fedha hizo zitapatikana kupitia Kampuni inayojishughulisha na masuala hayo katika Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Akizungumza na mwenyeji wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alikumbushia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi sita iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania katika Mfuko huo ikiwemo mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tabora-Kigoma-Msongati, Ujenzi wa Bwawa na Julius Nyerere, Mradi wa Umeme wa Benaco hadi Kyaka (220KV) mkoani Kagera, ujenzi wa nyumba 10,000 za makazi nafuu-Zanzibar, na mradi wa kuwezesha biashara ya usafirishaji na uingizaji wa bidhaa kutoka nje.

Aidha, Dkt. Nchemba, aliushukuru Mfuko huo kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi mil. 201 na dola za Marekani milioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi yenye urefu wa kilometa 51.1 kwa kiwango cha lami, barabara ambayo ujenzi wake umerejea baada ya kukwama kwa muda mrefu.

“Maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kwamba barabara hii ikamilike mapema ili kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote mbili wakiwemo wananchi watakaoitumia barabara hiyo, na wabunge wa mkoa wa Kigoma wanaisubiri kwa hamu barabara hiyo” Alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alimweleza Kiongozi huyo kuwa Tanzania imefungua milango kwa wawekezaji mbalimbali wakiwemo wanaotoka Abu Dhabi, kwenda kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miradi ya kimkakati, kilimo, mifugo, uvuvi na ujenzi wa nyumba katika sekta za elimu, afya, kilimo na mifugo.

“Tumefurahi kwa kutuahidi kuwa miradi yetu mikubwa ya kimkakati ya kuzalisha umeme, reli ya kisasa, mmeichukua na kuipeleka Serikalini na kwenye sekta binafsi, tuo tayari kushirikiana nao na kwa upande wa kilimo na mifugo, nawahakikishia kuwa ardhi ipo ya kutosha” alieleza Dkt. Nchemba

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, alisema kuwa ahadi hiyo ni matunda ya kusainiwa kwa Mkataba wa kutotoza kodi mara mbili kwenye mapato ya faida pamoja na udhibiti wa ukwepaji kodi uliosainiwa juzi kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu, mjini Dubai.