Jumatatu , 13th Aug , 2018

Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Liwale mkoani Lindi, Zuberi Kuchauka kupitia chama cha CUF amejivua nyadhifa zote ikiwemo ubunge na kujiunga na chama cha mapinduzi CCM.

Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Liwale (CUF), Zuberi Kuchauka.

Kuchauka ametangaza uamuzi huo leo Agosti 13, 2018 alipokaribishwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally katika ofisi ndogo za CCM zilizoko Lumumba jijini Dar es salaam.

Akizungumzia sababu za kurejea CCM, Kuchauka amesema ameamua kurejea CCM kwa sababu chama chake kimekuwa na mgogoro kwa muda mrefu hivyo kimepoteza dira, hali inayompa shida katika majukumu yake kwa wananchi.

"Kuanzia sasa hivi mimi sio mwanachama wa CUF kwa mtazamo huo maana yake ni kwamba, niliwahi kuwa CCM nimerejea. Narejea kwa sababu nina uhakika nimefanya utafiti wa kutosha na kubaini kuwa CCM ya Rais John Magufuli imerejea kwenye misingi ya TANU, na mimi kama mwananchi mpenda maendeleo sikuona kigugumizi kurejea," amesema Kuchauka.

Pia ameongeza; "Kwa nini nimechukua uamuzi huu leo, mnafahamu nilikuwa CUFnamna gani tumepoteza mwelekeo, mimi nimechaguliwa na wananchi, ninapokuwa huku kuna migogoro inanizuia kufanya kazi, CCM wametufanyia mambo makubwa sana. Ndio maana nimeona bora nirejee."

Naye Dkt. Bashiru amesema CCM itaendelea kupokea wanachama wapya na wanaorejea CCM, "Tunaendelea kupokea wanachama wapya na wanaorudi. Leo tumepokea wa upinzani akiwa mbunge Kuchauka wa CUF Liwale  anajiunga tena na CCM sababu aliwahi kuwa mwanaccm," amesema.

CUF imekumbwa na mgogoro tangu Profesa Ibrahim Lipumba kurejea katika uongozi mwaka 2016, ikiwa ni mwaka mmoja tangu alipojiuzulu uenyekiti wa chama hicho.