Ijumaa , 23rd Feb , 2018

Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Kenya Uhuru Muigai Kenyatta wamewaagiza Mawaziri wa Tanzania na Kenya kutatua tofauti ndogondogo zinazojitokeza katika biashara kati ya nchi hizo mbili.

Marais hao wametoa maagizo hayo leo asubuhi tarehe 23 Februari, 2018 walipokutana na kufanya mazungumzo katika hoteli ya Munyonyo mjini Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Dkt. Magufuli na Rais Kenyatta wamesema wanataka kuona biashara kati ya Tanzania na Kenya inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo bila vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti zilizojitokeza katika baadhi ya bidhaa zimalizwe.

“Kuna mambo madogo madogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote Mawaziri wa Kenya na Mawaziri wa Tanzania wakae kuyatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogo madogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawa sawa” amesema Rais Magufuli na kuungwa mkono na Rais Kenyatta.

Wametoa maagizo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya Mhe. Peter Munya.