Jumatatu , 22nd Aug , 2022

Magari matano ya kusafirisha mafuta na mizigo, yameteketea kwa moto ambao chanzo chake hakijulikani, uliozuka katika eneo la Chimala Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya

Moto huo ambao uliozuka usiku wa kuamkia leo Jumatatu Agosti 22/2022 uliteketeza pia nyumba tano za wananchi wa eneo hilo 

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbarali,  Reuben Mfune  amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo mpaka sasa hakijulikani

Amesema moto huo umesababisha hasara kubwa ya kuteketeza magari yaliyokuwa na shehena za mafuta, mizigo pamoja na nyumba zilizokuwa karibu na eneo hilo na kwamba thamani halisi ya mali zilizoteketea bado haijajulikana kutokana na udharura wa tukio hilo

Amesema  hadi sasa hakuna mtu aliyepoteza maisha katika ajali hiyo licha ya kwamba mtu mmoja ambaye alikuwa anasaidia kuokoa mali kuungua kwenye unyayo

 “Moto huo ulizuka majira ya saa tano usiku  na kuteketeza magari matano  na  kuunguza mali na samani zilizokuwa kwenye nyumba tano zilizokuwa karibu na eneo hilo na tunamshukuru mungu madhara kwa binadamu sio makubwa,” ameeleza Mfune.

Ameongeza kuwa gari la zimamoto lilifika katika eneo la tukio saa 7:00 usiku lakini magari manne yalikuwa tayari yameshateketea na hivyo likatumika kuzima gari moja ambalo pia kwa sehemu lilikuwa limeteketea kwa sehemu kubwa.

Amedai  kuwa chanzo cha moto kinahisiwa kuwa ni  baadhi ya watu kujaribu kuiba mafuta kwenye magari yaliyokuwa yameegeshwa katika eneo hilo  na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi cha moto huo.

Alitoa tahadhari kwa wananchi wa eneo hilo kuepuka kusogelea moto bila tahadhari kwa maelezo kuwa moto ni hatari na kwamba kuna uwezekano likatokea tatizo kama ilivyotokea Morogoro ambalo watu wengi walifariki